Bwana Yesu, nisaidie.
Yesu, Mwokozi wangu, nipe neema ya kukupenda ndani yangu, ili niweze kujifunza kukupenda wewe uishiye ndani ya wengine. Fungua macho yangu, Yesu, ili niweze kukuona ndani ya moyo wangu, nipate kutambua uwepo wako katika kila mtu ninayekutana naye. Yesu wangu, nipe neema ya kuona uzuri wako ndani yangu, ili niweze pia kuona uzuri wako ndani ya wengine.
Yesu wangu, nipe neema ya kupenda na kuthamini kazi yangu, ili niweze kufurahia na kuthamini kazi inayofanywa na wengine. Yesu, Mwokozi wangu, nipe neema ya kuhisi nguvu ya Msalaba wako Mtakatifu ndani yangu, ili niweze kila wakati kukutumainia. Yesu, Bwana wangu, nipe neema ya kujisamehe, ili moyo wangu uwe huru kusamehe wale walionikosea.
Kwa maana ikiwa siwezi kukupenda ndani yangu, Yesu wangu, inaniwia vigumu kukupenda kwa wengine. Ikiwa siwezi kukuona ndani yangu, Mwokozi wangu, inakuwa vigumu kukuona kwa wengine. Ikiwa siwezi kutambua uzuri wako ndani yangu, Mungu wangu, inaniwia vigumu kutambua uzuri wako kwa wengine. Na ikiwa siwezi kujisamehe, inaniwia vigumu kusamehe wale walioniumiza. Fungua macho ya moyo wangu, Yesu wangu, ili niweze kuona uzuri wa uumbaji wako kila mahali. "Ee Bwana, unifanye niwe chombo cha amani yako." Amina.