Skip to Content

MUNGU NI MSAADA WETU

21 Aprili 2026 na
MUNGU NI MSAADA WETU
Sr. Violet Kwanungu LSOF

Kuna nyakati katika maisha tunajisikia hatuna msaada kabisa, wakati matatizo yanatuzunguka kama jiwe zito tusiloweza kuliondoa. Katika nyakati kama hizo, ni rahisi kufikiri kwamba hakuna msaada unaokuja. Lakini Neno la Mungu linatukumbusha vinginevyo.

(Isaya 58:9) tunasikia ahadi yenye nguvu: “Ndipo utaiita, na Bwana ataitika; utalia, naye atasema, ‘Mimi hapa!” Ni faraja kubwa kujua kwamba Mungu hayuko mbali. Anasikia kila kilio, kila machozi ya kimya, na kila mzigo tunaoubeba tunapomwita, anaitika.

Changamoto za maisha haziji ili kutuangamiza, badala yake, zinakuja ili kutuvuta karibu zaidi na Mungu. Mara nyingi tunajaribu kubeba kila kitu kwa nguvu zetu wenyewe. Lakini kuna mizigo ambayo ni mizito sana kama jiwe, linazuia njia ya maisha yetu hatuwezi kuliondoa kwa mikono yetu, tunahitaji msaada wa Mungu kama mzaburi anavyotuambia. (Zaburi 121:2): “Msaada wangu u katika Bwana, aliyezifanya mbingu na nchi.” Yeye aliyeumba mbingu na nchi ana uwezo wa kushughulikia kila kinachotulemea maishani mwetu.

Hata pale tusipoelewa tunachopitia, tunapaswa kukumbuka kwamba Mungu ana kusudi. Katika (Isaya 43:19), anasema: "Tazama, nitatenda neno jipya; sasa litachipuka; je! Hamtalijua sasa? Nitafanya njia hata jangwani, na mito ya maji nyikani.” Hii ina maana hakuna hali iliyo kavu sana, iliyovunjika sana, au isiyo na tumaini ambayo Mungu hawezi kuibadilisha. Pale tunapoona jangwa, Mungu anaona mahali pa mito kutiririka.

Kwa hiyo, tusiruhusu changamoto zitukatishe tamaa bali zitusogeze karibu na Mungu. Ziimarishe imani yatu na pia zitukumbushe kwamba hatuko peke yatu.

Leo, mzigo wowote unaoubeba, ulete mbele za Bwana. Mtumaini na shikamana naye kwa sababu katika kila dhoruba, Mungu bado ni msaada wako, nguvu zako, na njia yako pekee ya kupata ushindi. Amina.

katika Blogu yetu
MUNGU NI MSAADA WETU
Sr. Violet Kwanungu LSOF 21 Aprili 2026
Shiriki posti hii
Lebo
Maktaba