"Mwanangu, uchume maarifa tangu ujana hata kuwa mwenye mvi, nawe utapata hekima." (Yoshua Bin Sira 6:18)
Fanya kile ambacho wengine hawafikirii kufanya: Kila siku fikiria jambo zuri la kufanya litakalokupa amani na furaha ya kweli moyoni mwako. Fanya kile ambacho wengine hawapendi kufanya: Fanya yale ambayo wengi hawavutiwi kuyafanya mambo ya kawaida yasiyoonekana wala kujulikana.
Fanya kile ambacho wengine hawana muda nacho kukifanya: Tumia muda wako vizuri fanya yale yatakayokusaidia kuleta mabadilko chanya maishani mwako. Fanya kile ambacho kitakupa amani moyoni mwako: Usilazimishe kufanya mambo yatakayopelekea uhisi maumivu moyoni fanya yale ambayo yanakuletea amani, furaha na utulivu moyoni mwako.
Fanya kile ambacho hakitaharibu amani ya watu: Sio kila jambo litawafurahisha watu wote na wala sio kila jambo litawachukiza watu wote. Fanya jambo sahihi ambalo litaleta amani ndani yako. Fanya kile ambacho utakifurahia baadaye: Ukipanda yaliyo mema utavuna matunda mema ambayo utayafurahia baadaye.
Ukithamini ulichonacho, Mungu atakipa uthamani wa kile unachokithamini: Kuthamini kitu tulichonacho ni pamoja na kukipenda na kukitunza kama zawadi nzuri za Mungu kwetu. Tukithamini kidogo tulicho nacho, tutathamini kikubwa walichonacho wengine, tusipothamini kikubwa tulichonacho kamwe hatutathamini kidogo walichonacho watu wengine.
“Ee Bwana,
unijulishe njia zako, unifundishe mapito yako. Uniongoze katika kweli yako na
kunifundisha, maana Wewe ndiwe Mungu wa wokovu wangu; nakungoja Wewe mchana
kutwa.” (Zaburi 25:4-5)