Baba yetu mpendwa, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, kwa kweli tutakukumbuka kwa mambo mengi mazuri na ya kupendeza uliyofanya hapa duniani kwa ajili ya Shirika letu, kwa ajili ya Kanisa, na kwa ajili ya Taifa letu. Popote ulipokanyaga, uliacha alama isiyofutika katika mioyo ya watu wa kila aina: wazee, vijana, watu wazima, watoto, maskini, viongozi, wasomi na wasio na elimu.Uwepo wako umeiachia dunia historia itakayokumbukwa kizazi na kizazi. Wewe ulikuwa taa iliyowaka na kuwaangazia watu wengine. Wewe ulikuwa kitabu kilichosomwa na watu bila ya wewe mwenyewe kujua na tutaendelea kusoma kitabu cha maisha yako. Uwepo wako duniani umeleta baraka kwa watu, uwepo wako umeleta faraja, uwepo wako umeleta maendeleo kwa wengine.
Muunganiko wako na Mungu ulikuwa kama gari na injini; uhusiano wako na Mungu ulikuwa kama samaki ndani ya maji; muunganiko wako na Mungu ulikuwa kama simu na betri; muunganiko wako na Mungu ulikuwa kama mti wa mzabibu na matawi yake, kama Yesu anavyosema. "Mimi ni mzabibu, ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lolote." (Yohana 15:5) Uliishi maisha ya kawaida kwa nje, lakini ndani yako ulibeba kitu kisicho cha kawaida, ukagusa maisha ya watu wengi. Ulikuwa kama nyota iliyoangaza usiku, na wala mwangaza wake haukuweza kuzimika. Ulitumia vyema karama ulizojaliwa na Mwenyezi Mungu, ili kuwafaidisha wengini. Umekuwa wakili mwaminifu kama Yesu anavyosema. "Ni yupi basi wakili mwaminifu na mwenye busara, ambaye bwana wake atamfanya msimamizi juu ya watumishi wake wote, ili awape watumishi wengine chakula chao wakati unaofaa? Heri mtumishi yule ambaye bwana wake atakaporudi atamkuta akifanya hivyo.” (Luka 12:42-43) Pumzika kwa amani baba yetu. Amina